Barker amekiri kuwa haitakuwa mechi rahisi ndio maana amewaandaa wachezaji kuhakikisha tunacheza vizuri ili kuweza kupata alama tatu muhimu ugenini.
Barker ameongeza kuwa baada ya timu kurejea kutoka jijini Arusha jana wachezaji wamefanya mazoezi asubuhi na wote wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo wa kesho.
"Tumejipanga kuendelea kucheza soka safi na kupata alama tatu kwenye mchezo wa kesho, ni wazi haitakuwa mechi nyepesi lakini tumejiandaa kwa hilo. Tunawaheshimu Namungo lakini dhamira yetu ushindi," amesema kocha Barker.
Kwa upande wake mlinzi wa kushoto, Anthony Mligo amesema pamoja na ugumu na upinzani ambao tunatarajia kukutana nao kutoka kwa Namungo lakini tumejipanga na tupo tayari kupambana mpaka mwisho ili kupata alama tatu.
"Tunaamini tunaenda kukutana na mechi ngumu, Namungo ni timu imara ina wachezaji wazoefu pamoja na kocha bora, lakini tutaingia uwanjani kwa mpango mzuri tutakaolekezwa na walimu, tunawaahidi mashabiki wetu kupata alama tatu muhimu ugenini," amesema Mligo.