Simba Sports Club

Tupo tayari kuivaa Geita Gold Leo

31 Aug 2026

Leo saa 12:30 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuikabili Geita Gold katika mchezo wa tano wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027.

Mchezo wa leo ni wa pili katika Uwanja wa nyumbani baada ya ule wa Alhamisi tulioibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya Coastal Union.

Nafasi za timu zote kwenye msimamo....

Tupo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC tukiwa na alama 12 na mabao saba baada ya kupata ushindi kwenye michezo yote minne tuliyocheza tukiwa na ushindi wa asilimia 100.

Kwa upande wapinzani wetu Geita Gold wapo nafasi ya tano kwenye msimamo wakiwa na alama saba baada ya kushinda mechi mbili kutoka sare moja na kupoteza moja.

Tulivyokutana mara ya mwisho....

Geita imepanda daraja msimu huu baada ya kupita miaka miwili ambayo walikuwa wakishiriki Ligi daraja la kwanza 'Championship'.

Mara ya mwisho kukutana na Geita ilikuwa msimu wa 2023/2024 ambapo tuliwafunga katika mechi zote mbili. Mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Februari 12/2024 katika Uwanja wa CCM Kirumba tukaibuka na ushindi wa bao moja.

Mchezo wa mzunguko wa pili ulipigwa Mei 21/2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tukaibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Advertisement

Hali ya Kikosi....

Mlinzi wa kulia, David Kameta 'Duchu' atakosekana kwenye mchezo wa leo baada ya kupata maumivu katika mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union.

Mbali na Duchu tutaendelea kuwakosa Shomari Kapombe na Nickson Kibabage ambao ni majeruhi huku Ibraheem Jabaar na Anthony Mligo wakiendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Habari njema ni kwamba kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma ambaye alikosekana katika mechi mbili zilizopita amerejea kikosini na kama mwalimu ataona inafaa ataweza kumtumia katika mchezo wa leo.

Wachezaji wakuchungwa.....

Libbase Gueye, Anicet Oura, Elie Mpanzu na Clatous Chama ni nyota ambao wanatarajiwa kuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Geita Gold kwenye mchezo wa leo.

Kwa upande wa Geita Gold nyota wao wa kuchungwa ni mshambuliaji, Obrey Chirwa aliyefunga mabao manne, Richardson Ngondya na Yusuph Mhilu wenye mabao mawili kila mmoja.

Matarajio ya jinsi mechi itakavyokuwa......

Mchezo unatarajiwa kuwa wakuvutia kutokana na aina ya soka kwa pande zote lakini tuna nafasi ya zaidi ya asilimia 70 kupata alama zote tatu ingawa ni wazi kuwa haitakuwa kazi rahisi.