Simba Sports Club

Tupo tayari kuikabili Coastal Union Kesho

26 Aug 2026

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo saa moja usiku yamekamilika.

Matola amesema haijawahi kuwa mechi nyepesi baina ya Simba na Coastal na mara zote wamekuwa wakitupa ushindani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

Matola ameongeza kuwa suala la wachezaji wetu kupata kadi nyekundu tatu kwenye mechi tatu zilizopita linaendelea kufanyiwa kazi mazoezini kwakuwa sio jambo zuri kwa walimu na wamekuwa wakiwasisitiza wachezaji kuwa makini hasa baada ya uwepo Football Video Support (FVS).

Advertisement

"Ni mechi yetu ya kwanza ya nyumbani, tunafahamu Coastal Union haijapata ushindi kwenye mechi zake zilizopita lakini wamekuwa wakicheza soka safi ndio maana tutaingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari zote na lengo ni kupata alama tatu," amesema Matola.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, mlinda mlango, Hussein Abel amesema kila kitu sawa na kila mmoja yupo tayari kuhakikisha anaipambania timu kupata alama tatu muhimu za nyumbani.

"Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo wa kesho pamoja na ugumu tutakaokutana nao lakini tupo tayari kuwapa furaha mashabiki wetu," amesema Hussein Abel.