Timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens imepoteza mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya michuano ya CAF Womens Champions League CECAFA Qualifiers 2026 dhidi ya Kenya Polisi uliopigwa Uwanja wa Pele Kigali kwa mabao 2-1.
Kenya Polisi walipata bao kwanza dakika ya 17 kupitia kwa Faith Mboya aliyepiga shuti la chini chini lililomshinda mlinda mlango, Ruth Aturo.
Baada ya bao hilo bado Polisi Kenya waliendelea kuwa bora lakini kuanzia dakika ya 25 Simba Queens ilirejesha umailiki wa mchezo mpaka timu zinaenda mapumziko.
Kipindi cha pili Queens ilirejea kwa kasi ambapo kiungo mshambuliaji, Senaf Demis alitupatia bao la kusawazisha dakika ya 69 baada ya shuti la Vivian Corazone kumshinda mlinda mlango wa Polisi kabla ya kumkuta mfungaji.
Martha Emedotz aliipatia Polisi Kenya bao la pili dakika ya 78 baada ya kutokuwa na maelewano mazuri baina ya mlinzi wa kushoto Aisha Omary na mlinda mlango Ruth Aturo.
Matokeo haya yanaifanya Simba Queens kusubiri matokeo ya mwisho ya mchezo kati ya Polisi Kenya dhidi ya Top Girls ili kuweza kufahamu kama wataweza kufuzu hatua inayofuata au watakuwa wameaga mashindano.