Leo saa 10:15 jioni kikosi kitashuka katika Uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Pamba Jiji katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC.
Nafasi za timu zote kwenye msimamo....
Tupo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC tukiwa na alama tatu na mabao mawili baada ya kupata ushindi wa 2-0 tuliopata dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja Kaitaba, Agosti 16.
Kwa upande wapinzani wetu Pamba wapo nafasi ya 12 kwenye msimamo wakiwa na alama moja kufuatia kulazimishwa sare ya bao moja na Dodoma Jiji katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Agosti 15.
Msimu uliopita tulivyokutana.....
Mchezo wa pili ulipigwa Juni 14/2026 katika Uwanja wa KMC Complex na tukaibuka na ushindi wa mabao 2-1. Mabao yetu yalifungwa na Elie Mpanzu na Libasse Gueye huku la Pamba Jiji likifungwa na Methew Tegisi.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Machi 19/2026 katika Uwanja wa CCM Kirumba na kumalizika kwa sare ya kufungana bao moja. Bao letu lilifungwa na Anicet Oura wakati la Pamba lilifungwa na James Mwashinga.
Mabadiliko na Majeruhi.....
Mlinda mlango wetu namba moja, Djibrilla Kassali ataukosa mchezo kutokana na kupata maumivu ya goti kwenye mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar na Hussein Abel anatajiwa kuanza katika mechi ya leo.
Kiungo mkabaji Yusuph Kagoma nae alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Kagera lakini yeye ni 50/50 anaweza kucheza au apumzishwe ili kumfanya kuwa fiti zaidi.
Kwa upande wa Pamba Jiji wao hawajasema watamkosa nani huku nyota wao ambao walikosekana mechi ya kwanza kutokana na kukosa vibali wamevipata na wapo tayari kushuka dimbani.
Matarajio ya jinsi mechi itakavyokuwa......
Mchezo unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu zote kutokana na usajili uliofanywa na pande zote lakini tuna nafasi kubwa ya kupata alama tatu kwa sababu ya ubora wa kikosi tulionao ingawa ni wazi haitakuwa rahisi.