Leo saa 12 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Airtel mkoani Singida kuikabili Singida Black Stars katika mchezo wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027.
Nafasi za timu zote kwenye msimamo....
Tupo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC tukiwa na alama sita na mabao manne baada ya kupata ushindi wa 2-0 tuliopata dhidi ya Kagera Sugar na baadae 2-1 dhidi ya Pamba Jiji.
Kwa upande wapinzani wetu Singida Black Stars wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na alama nne kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate kwenye mchezo wa kwanza nyumbani kabla kulazimishwa sare ya bao moja na Kagera Sugar katika mchezo wa pili uliopigwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Msimu uliopita tulivyokutana.....
Msimu uliopita tulipata alama sita mbele ya Singida Black Stars baada ya kuwafunga mechi zote mbili.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Machi 11/2026 katika Uwanja wa Airtel na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Mabao yetu yakifungwa na Anicet Oura na Elie Mpanzu wakati lile la Singida likifungwa na Mossi Ndumumwe.
Mchezo wa mzunguko wa pili ulipigwa Juni 27/2027 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na tukaibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Anicet Oura na Elie Mpanzu.
Mabadiliko na Majeruhi.....
Tutaendelea kuwakosa Shomari Kapombe na Nickson Kibabage ambao ni majeruhi wakati David Kameta 'Duchu' na Ibraheem Jabaar wakiendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Mlinda mlango Djibrilla Kassali ambaye alipata maumivu ya goti kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar jana amefanya mazoezi pamoja na wenzie tunasubiri kuona kama kocha atampa nafasi au ataendelea na Hussein Abel ambaye alifanya vizuri mechi iliyopita dhidi ya Pamba Jiji.
Kwa upande wa Singida Black Stars kiungo wao mkabaji Mohamed Damaro ambaye msimu uliopita alicheza Yanga kwa mkopo amerejea kikosini na anataraji kuwepo kikosini kwenye mchezo wa leo kutokana na ukubwa na umuhimu wake.
Wachezaji wakuchungwa.....
Libbase Gueye, Anicet Oura, Elie Mpanzu na Clatous Chama ni nyota ambao wanatarajiwa watakuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Singida Black Stars kwenye mchezo wa leo.
Kwa upande wa Singida Black Stars washambuliaji wao Jonathan Sowah na Methew Tegisi ndio nyota wakuchungwa zaidi ambao wametupia kambani mabao matatu kati ya manne waliyofunga kwenye mechi mbili zilizopita.
Matarajio ya jinsi mechi itakavyokuwa......
Mchezo unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu zote kutokana na ubora na pande zote lakini Simba tuna nafasi kubwa ya kupata alama tatu kutokana na rekodi kuwa bora kwetu kila tunapokutana na Singida.
N.B Katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Kagame tulipokutana kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali Julai 31/2026 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Mabao yetu yalifungwa na Ibrahim Doumbia na Elie Mpanzu wakati lile la Singida Black Stars likifungwa na Methew Tegisi.