Simba Sports Club

Queens yaichapa Top Girls

22 Aug 2026

Timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Top Girls kutoka Burundi katika mchezo wa CAF Womens Champions League CECAFA Qualifiers 2026 uliopigwa Uwanja wa Pele jijini Kigali nchini Rwanda.

Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu na kufanya mashambulizi kadhaa lakini dakika zote 45 za kipindi cha kwanza hakuna aliyefanikiwa kupata bao.

Kipindi cha pili Top Girls walirudi kwa kasi ambapo dakika ya 58 walikosa mkwaju wa penati uliopigwa na Asha Djafar baada ya mchezaji wetu kushika mpira ndani ya 18.

Mshambuliaji Aisha Mnunka alitupatia bao la kwanza dakika ya 68 baada ya kupokea pasi kutoka nyuma na kuwazidi ujanja walinzi wa Top Girls.

Advertisement

Kasamfula Rida alitupatia bao la pili dakika ya 71 baada ya kupokea pasi safi kutoka nyuma pia na kupiga shuti lililomshinda mlinda mlango wa Top Girls.

Kocha Mussa Hassan Mgosi alifanya mabadiliko ya kuwatoa Vivian Corazone, Zainah Nandede, Hellen Kutsanedzi na Aisha Mnunka na kuwaingiza Kasamfula Rida, Fatuma Issa, Senafu Wakuma na Elizabeth Nashon.

Simba Queens itashuka tena dimbani Jumatatu Agosti, 24 saa saba mchana kuikabili Kenya Polisi katika mchezo wa pili wa michuano hii.