Leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuikabili Coastal Union katika mchezo wa nne wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027.
Nafasi za timu zote kwenye msimamo....
Tupo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC tukiwa na alama tisa na mabao sita baada ya kupata ushindi wa 2-0 tuliopata dhidi ya Kagera Sugar, 2-1 dhidi ya Pamba Jiji pamoja na 2-1 dhidi ya Singida Black Stars.
Kwa upande wapinzani wetu Coastal Union wapo nafasi ya 14 kwenye msimamo wakiwa na alama moja kufuatia kupoteza mechi mbili na kutoka sare moja.
Msimu uliopita tulivyokutana.....
Msimu uliopita tulipata alama sita mbele ya Coastal Union baada ya kuwafunga mechi zote mbili.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Aprili 2/2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Mabao yetu yakifungwa na Seleman Mwalimu na Ismail Toure.
Mchezo wa mzunguko wa pili ulipigwa Mei 21/2026 katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga na tukaibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Libasse Gueye na Anicet Oura wakati lile la Coastal likifungwa na Maabad Maulid.
Mabadiliko na Majeruhi.....
Tutaendelea kuwakosa Shomari Kapombe,Nickson Kibabage na Yusuph Kagoma ambao ni majeruhi wakati Ibraheem Jabaar na Anthony Mligo wakiendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Mlinzi wa kulia David Kameta 'Duchu' amerejea kikosini baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji.
Kwa upande wa Coastal Union kocha wao mkuu, Fikiri Elias ameweka wazi kuwa wanafahamu mapungufu yetu watapigana kupata alama tatu.
Wachezaji wakuchungwa.....
Libbase Gueye, Anicet Oura, Elie Mpanzu na Clatous Chama ni nyota ambao wanatarajiwa watakuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Coastal Union kwenye mchezo wa leo.
Kwa upande wa Coastal Union mshambuliaji wake Maabad Maulid ndiye nyota anayetazamwa zaidi kuiongoza safu ya ushambuliaji ya 'Wagosi wa Kaya' hao.
Matarajio ya jinsi mechi itakavyokuwa......
Mchezo unatarajiwa kuwa wakuvutia kutokana na aina ya soka kwa pande zote lakini tuna nafasi kubwa ya kupata alama tatu kutokana na rekodi kuwa bora upande wetu kila tunapokutana na Coastal Union.