Timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii baada kuibuka na ushindi wa bao moja dhidi JKT Queens uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex.
Mlinzi wa kulia, Zainah Nandede alishindwa kuendelea na mchezo na kufanyiwa mabadiliko dakika ya 21 baada ya kupata maumivu nafasi yake ikachukuliwa na Violeth Nicholas.
JKT Queens ilicheza pungufu kwa takribani dakika 30 baada ya mlinzi wa kati, Esther Maseke kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 60 baada ya kumchezea madhambi, Aisha Mnunka.
Aisha Mnunka alitupatia bao la kwanza dakika ya 62 baada ya kumalizia pasi ndefu iliyopigwa kutoka katikati ya uwanja na Fasila Adhiambo
Kocha Mussa Mgosi alifanya mabadiliko ya mchezaji mmoja pekee ambapo alimtoa Vivian Corazone na kumuingiza Neema Mtunzi dakika ya 89.
Mchezo huu umeashiria kufunguliwa rasmi kwa pazia la Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL) msimu mpya wa 2026/2027.