Naibu Waziri wa Fedha, Mh. Laurent Deogratius Luswetula amesema Serikali itaendelea kutoa mchango mkubwa katika masuala mbalimbali ya kuinua michezo nchini.
Mh. Luswetula ameyasema hayo baada ya kushiriki Simba Marathon 2026 katika Fukwe za Coco ambapo amewapongeza Viongozi wa klabu kwakuja na wazo hilo huku akisema Serikali itakuwa tayari kutoa mchango wowote utakaohitajika ili kusaidia kuinua vipaji.
"Kwanza niwapongeze Viongozi kwa kuja na wazo hili la Marathon nasi kama Serikali tunaahidi tutaendelea kuwashika mkono ili kuzidi kuinua vipaji vya michezo," amesema Mh. Luswetula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori amesema mwaka huu tunaadhimisha miaka 90 ya kuanzishwa klabu yetu lakini kuanzia sasa Simba Marathon itakuwa inafanyika kila mwaka.
"Rais wa Heshima wa klabu, Mohamed Dewji 'Mo' amesema yupo tayari kuweka pesa kwa ajili ya Simba Marathon na ninatangaza rasmi tutakuwa tunafanya kila mwaka na mwakani itakuwa kubwa mara 10 ya hii ya leo," amesema Rweyemamu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Chama cha Riadha Tanzania (RT), Alfredo Shahanga amewapongeza Viongozi kwakuja na wazo hili huku akisema wataendelea kushirikiana nasi kwenye Marathon kwani baada ya miaka michache mbele yatakuwa mashindano makubwa ndani na nje ya nchi.
Nae Mtendaji Mkuu wa klabu, Bi. Zubeda Sakuru amewashukuru wadhamini wote walioshiriki pamoja nasi pamoja na mashabiki waliojitokeza kitu ambacho kimetupa moyo na tukifahamu mwakani itakuwa kubwa zaidi.
"Tunawashukuru wote mliotuunga mkono na jambo tunalowaahidi mwakani Marathon hii itakuwa kubwa zaidi," amesema CEO, Zubeda.