Uongozi wa klabu kupitia Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally umetangaza rasmi kuwa Simba Day ya mwaka huu itafanyika Agosti 8 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ahmed amesema Simba Day ya mwaka huu ambayo itakuwa inatimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake itakuwa ya tofauti na zilizopita hivyo kila Mwanasimba hatakiwi kuikosa.
Ahmed amesema kwakuwa safari hii Simba Day itafanyika Uwanja wa Uhuru ambao sio mkubwa kama ilivyo Benjamin Mkapa kila Mwanasimba atakayetaka kushiriki Simba Day lazima akate tiketi mapema ili kupunguza usumbufu.
"Kumekuwa na tetesi nyingi kuhusu Simba Day ya mwaka huu lakini leo tunawatangazia rasmi kuwa Simba Day itafanyika Agosti 8 katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam," amesema Ahmed.
Hivi hapa Viingilio:
Platinum Shilingi 250,000
Vip A Shilingi 100,000
Mzunguko Shilingi 20,000
Tayari tiketi zimeanza kuuzwa kwa njia ya mitandao na pia kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam huku Wanasimba wakitakiwa kununua mapema ili kuepuka usumbufu.