Simba Sports Club

Ni kufa au kupona Dabi ya Kariakoo Leo

10 Oct 2026

Leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kuikabili Yanga katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo ukiwa ni mzunguko wa Saba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027.

Kariakoo Dabi ni moja ya mechi ngumu ambayo mara nyingi imekuwa ikivuta hisia za mashabiki wengi ndani na nje ya nchi.

Nafasi za timu zote kwenye msimamo....

Tupo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC tukiwa na alama 18 na mabao 11 baada ya kupata ushindi kwenye michezo yote sita tuliyocheza tukiwa na ushindi wa asilimia 100.

Kwa upande wapinzani wetu Yanga wao ndio vinara wakiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo na alama 18 sawa nasi lakini wakiwa na uwiano mzuri wa mabao yakufunga wakiwa wamefunga 16.

Tulivyokutana mara ya mwisho....

Msimu huu tayari tumekutana mara moja katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam Agosti 12 na kupoteza kwa bao moja.

Mchezo huo ulikuwa mkali muda wote huku timu zikigawana nyakati za kutawala mchezo na bao pekee lililotengeneza mechi likifungwa na Albert Kangwanda.

Hali za Vikosi....

Advertisement

Kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri ambapo wachezaji ambao walikuwa majeruhi kama nahodha, Shomari Kapombe na mlinzi wa kushoto Nickson Kibabage wako tayari kwa mchezo wa leo.

Mchezaji pekee ambaye bado hajaanza mazoezi ni mlinda mlango, Yakoub Mohamed huku walinzi Wilson Nangu na Abdulazak Hamza wakiwa kwenye hatua za mwisho za kurejea rasmi dimbani.

Kwa upande wa wapinzani wetu Yanga watamkosa nyota wao Stephen Aziz Ki anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Geita Gold.

Nahodha wao, Dickson Job na mshambuliaji, Clement Mzize wao afya zao zimeimarika na wanaweza kuwa sehemu ya mchezo wa leo kama kocha Manqoba Mngqithi ataona inafaa.

Wachezaji wakuchungwa.....

Libase Gueye, Anicet Oura, Elie Mpanzu na Clatous Chama ni nyota ambao wanatarajiwa kuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Yanga kwenye mchezo wa leo.

Kwa upande wapinzani wetu nyota wao wa kuchungwa ni Peter Shalulile, Albert Kangwanda, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya.

Matarajio ya jinsi mechi itakavyokuwa......

Mchezo unatarajiwa kuwa wakuvutia kutokana na aina ya soka kwa pande zote na wachezaji walionao na mbinu bora pekee ndizo zitafanya timu yoyote kupata alama tatu katika mechi ya leo.