Kocha mkuu, Steve Barker amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya NBC 2026/2027 dhidi ya Yanga yamekamilika na kila kitu kipo tayari.
Barker amesema mchezo utakuwa mgumu kwa kila kitu kutokana na maandalizi ya timu zote pamoja na aina wachezaji waliopo lakini tumejiandaa na tupo tayari kuwakabili.
Barker ameongeza kuwa lengo letu la kwanza kwenye mchezo wa kesho ni kushinda na kutwaa taji ingawa haitakuwa rahisi.
"Sisi tumejiandaa kwa mchezo wa kesho na tupo tayari kimwili na kiakili kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii. Tutaingia kwenye mchezo huo kwa lengo moja tu kuhakikisha tunashinda na kuchukua taji," amesema Barker.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, mlinzi wa kushoto, Nickson Kibabage amesema wapo tayari kufuata maelekezo watakayopewa na mwalimu na kila mmoja yupo tayari kupambana kuiwezesha timu kupata ushindi.
"Sisi kama wachezaji tupo tayari kufuata maelekezo kutoka kwa walimu na lengo letu ni kuwapa furaha mashabiki wetu kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii," amesema Kibabage.