Kocha mkuu, Steve Barker amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Singida Black Stars utakaopigwa Uwanja wa Airtel saa 12 jioni yamekamilika na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri.
Barker amesema baada ya safari ya kutoka Mwanza mpaka Singida wachezaji walipumzika na leo jioni watafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kesho kushuka dimbani.
Barker ameongeza kuwa tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Singida lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata alama zote tatu.
"Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda na kupata alama zote tatu, haitakuwa mechi rahisi kutokana na ubora wa wapinzani lakini tumejipanga lengo ni ushindi," amesema Barker.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto, Anthony Mligo amesema pamoja na ugumu ambao tutaenda kukutana nao kesho lakini tumejiandaa vizuri kuwakabili na kuisaidia timu kupata ushindi.
"Singida ni timu ngumu na ina wachezaji bora lakini Simba ni timu kubwa na inaweza kucheza kwenye mazingira yoyote na lengo letu ni kupata alama tatu," amesema Mlingo.