Simba Sports Club

Alichosema kocha Barker kuelekea mchezo dhidi ya Mighty Wanderers

12 Sep 2026

Kocha Mkuu, Steve Barker ameweka wazi kuwa tutaingia kwenye mchezo wa kesho wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mighty Wanderers tukiwa na lengo moja la kupambana ili kupata ushindi.

Barker amesema tunapaswa kuingia tukiwa na morali ya hali ya juu hasa ukizingatia tunacheza nyumbani ambapo tunategemea mashabiki wetu watakuja kwa wingi kutupa sapoti nasi tunawaahidi tutajitoa kwa asilimia 100 ili kuwapa furaha.

"Ni muhimu kwetu kuingia uwanjani tukiwa na morali ya hali ya juu, tuna mazingira mazuri ya kupata matokeo chanya kwakuwa tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu ambao tunaamini watakuja kwa wingi kutupa sapoti."

Ni mchezo ambao ni lazima tushinde ili tusonge mbele na hilo ni jambo la kwanza lakini pia tunatakiwa kucheza soka safi ili kuwapa burudani mashabiki wetu watakaokuja kutuunga mkono," amesema kocha Barker.

Advertisement

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, David Kameta 'Duchu' amesema kila atayepata nafasi ya kucheza kwenye mchezo wa kesho atajitoa kwa asilimia 100 kuisaidia timu kupata ushindi.

Duchu amewaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu huku akiahidi watawalipa kwa kuonyesha kandanda safi na kupata ushindi.

"Mchezo wa kwanza kule Malawi hatukucheza vizuri sana ingawa tulipata ushindi lakini kesho tunataka kucheza soka safi na kupata ushindi ili kuwapa furaha Wanasimba."

"Kikubwa tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi sisi kama wachezaji tunawaahidi tutajitoa kwa asilimia 100 ili kupata ushindi," amesema Duchu.