Nahodha Msaidizi Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' amesema katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates utakaopigwa Aprili 24, tutaingia kwa kuwaheshimu na kuchukua tahadhari zote.
Zimbwe Jr amesema Orlando walicheza kwa kutuheshimu na kutumia muda mwingi kujilinda ili kuhakikisha hatuwafungi mabao mengi kitu ambacho tutakifanya tukienda kwao.
Mlinzi huyo wa kushoto ameongeza kuwa michuano ya kimataifa inawaongezea uzoefu kwa sababu wanakutana na wachezaji wakubwa ndiyo maana kila mwaka wanapambana kwenye ligi ya ndani ili kupata tiketi ya kushiriki.
"Tunajua Orlando wakiwa kwao hawachezi kama walivyocheza jana, wao walituheshimu nasi tukienda kwao tutawaheshimu. Ndoto ya kila mchezaji ni kuiona timu ikiingia nusu fainali," amesema Zimbwe Jr.
Nahodha huyo msaidizi pia amewashukuru mashabiki wetu kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani na walikuwa na mchango mkubwa katika ushindi tuliopata kutokana na sapoti waliyokuwa wanatoa.
"Kwa niaba ya wachezaji wenzangu nachukua nafasi hii kuwapongeza mashabiki wetu kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani. Nguvu yao imeonekana na mchango wao kwenye ushindi tuliopata ni mkubwa. Nawaomba waendelee kutuunga mkono sisi tutahakikisha tunawapa furaha," amesema Zimbwe Jr.