Magori ameyasema hayo mbele ya Waandishi wa Habari huku akiweka wazi kuna watu kwa makusudi wamedhamiria kutugawanya kwa ajili ya manufaa yao binafsi kitu ambacho kinatakiwa kifike mwisho.
“Lugha za kutugawanya sasa zifike mwisho. Tunaandaa mfumo wa utoaji wa kadi ambao utakuwa ni wa kisasa. Sisi ni klabu ambayo itakuwa na pesa nyingi kuliko klabu yoyote. Tunakwenda kutengeneza klabu yenye uongozi bora," amesema Magori.
Akizungumza kuhusu hali ya kikosi Magori amesema “Kiufundi timu iliyumba sababu kocha aliyeanza msimu aliondoka, akaja mwingine hatukukubaliana. Kitu kingine ambacho watu hawakisemi ni mechi ya ngao ya jamii beki muhimu wa kati aliumia, mechi inayofuata kipa namba moja akaumia. Tukiwa Mali beki muhimu mwingine wa kati ameumia lakini maneno yanakuzwa."
Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu, Murtaza Mangungu amesisitiza kuwa hakuna mgogoro wowote baina ya mwekezaji Mohamed Dewji 'Mo' pamoja na Viongozi na wala hakuna mgongano wa kimaslahi.
“Wanasema kuna mgogoro kati ya upande wa klabu na mwekezaji, mimi na Mwenyekiti wa Bodi tunaongea kila mara, kama ni Mo mimi mara ya mwisho niliongea nae jana saa nane mchana. Sisi hatuna jambo la siri, timu inafanya mipango yake kama kuna taarifa ya kutoka inatoka," amesema Mwenyekiti Mangungu.