Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-1 tuliopata dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Jumatano katika Uwanja wa Airtel.
Tunafahamu haitakuwa mechi rahisi, tunakutana na timu ambayo inaundwa na nyota wengi ambao wanauzoefu mkubwa wa Ligi Kuu lakini tupo tayari kupambana ili kupata alama tatu.
Maandalizi ya Mchezo yamekamilika.......
Kocha mkuu, Steve Barker amesema kikosi kikosi kipo tayari kwa mchezo na wachezaji wapo kwenye hali nzuri kwa ajili ya kupigania furaha ya Wanasimba katika dimba la Sheikh Amri Abeid.
Barker ameweka wazi furaha yake kutokana na maendeleo chanya ya kikosi chetu kinavyocheza kitu ambacho kinazidi kumpa matumaini ya kufanya vizuri.
"Kikosi chetu kinazidi kuimarika na tunahitaji kuendelea kupata ushindi kwenye mechi zetu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri, kuhusu mchezo tupo tayari na maandalizi yamekamilika," amesema kocha Barker.
Wapambanaji wetu wapo tayari.....
Kwa upande wake mlinzi wa kulia, David Kameta 'Duchu' amesema pamoja na ugumu na upinzani ambao tutakutana nao lakini tumejipanga na malengo yetu ni kupata alama tatu muhimu ugenini.
"Kwa upande wetu kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo, tunafahamu utakuwa mgumu na tunawaheshimu wapinzani wetu lakini tupo hapa kwa ajili ya kupambana hadi mwisho kupata alama tatu," amesema 'Duchu'.
Mwalimu aendelea kutumika adhabu....
Mshambuliaji Seleman Mwalimu ataikosa pia mechi ya leo kutokana na kuendelea kutumikia adhabu ukiwa ndio mchezo wake mwisho.
Mwalimu alifungiwa mechi tatu kutokana na matendo yasiyokubalika michezoni lakini adhabu hiyo inamalizika leo ambapo mchezo ujao dhidi ya Pamba Jiji atakuwa kikosini.