Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa kumbukumbu ya kupoteza mechi ya mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Disemba 7 mwaka jana.
Mchezo wa Dabi ya Mzizima mara zote unakuwa na upinzani wa asili na tupo tayari kuhakikisha sisi ndio tunafurahi baada ya filimbi ya mwisho.
Alichosema kocha Barker kuhusu Mzizima Dabi........
Kocha Mkuu, Steve Barker amesema ni mchezo muhimu kwakuwa unatoa taswira kwenye mbio za ubingwa ndio maana amewaandaa wachezaji kimwili na kiakili kuhakikisha tunapata ushindi.
Barker ameendelea kwa kusema kuwa Azam ni timu imara na inaundwa na wachezaji wengi wazoefu na kocha bora lakini tumefanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu.
Akizungumzia kuhusu hali ya wachezaji kocha, Barker amesema wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja anafahamu umuhimu wa ushindi kwakuwa malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu.
"Maandalizi ya mchezo yamekamilika, wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri. Tunategemea kupata ushindani mkubwa lakini tumejiandaa kuwakabili," amesema Barker.
Wachezaji wapo tayari kwa mchezo....
Nahodha wa timu, Shomari Kapombe amesema licha ya ubora walionao Azam lakini tupo kuhakikisha tunapambana mpaka mwisho ili kuhakikisha tunapata ushindi.
"Wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na morali ipo juu, sote tunafahamu Azam ni timu nzuri lakini tumejipanga na tupo tayari kuwakabili na kupata alama tatu muhimu," amesema Kapombe.
Ni mechi ya kisasi.......
Katika michezo 15 ya Ligi Kuu ya NBC tuliyocheza kwenye mzunguko wa kwanza tumepoteza mechi moja tu ambayo ilikuwa dhidi ya Azam FC tena tukiwa nyumbani Benjamin Mkapa.
Leo tunaenda Azam Complex tukiwa na dhamira moja ya kuhakikisha tunashinda ugenini na kulipa kisasi cha Disemba 7.