Simba Sports Club
News

Tupo tayari kwa Dabi ya Kariakoo

1 Mar 2026

Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa Ligi uliopita dhidi ya Dodoma Jiji ambao tulionyesha kiwango bora.

Dabi ya Kariakoo ni moja ya mechi inayotazamwa na maelfu ya mashabiki barani Afrika na lengo letu ni kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu wote kwa kupata ushindi.

Ni wazi kwamba hatujapata ushindi kwenye michezo sita ya Dabi ya Kariakoo iliyopita lakini leo ni tofauti, tuna kikosi kipya, benchi jipya la ufundi, pamoja na morali ya juu ili kufanikisha ushindi leo.

Barker awatoa presha wachezaji....

Kocha Mkuu Steve Barker amesema ili kushinda mechi kubwa kama hii tunapaswa kucheza kwenye kiwango bora na kupunguza makosa ambayo yanaweza kukugharimu pamoja na kutumia nafasi zitakazopatikana.

"Nimeongea na wachezaji na kuwasisitiza kutokuwa na presha kuelekea mchezo huu kutokana na matokeo ya nyuma tuliyopata dhidi yao badala yake tunapaswa kujiamini."

"Ili kushinda mechi kubwa kama hii tunapaswa kuwa kwenye kiwango bora na kutumia vizuri nafasi tutakazopata. Nafikiri tuna nafasi ya kufanya vizuri," amesema Barker.

Kapombe nae afunguka.....

Advertisement

Kwa upande wake nahodha, Shomari Kapombe amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 na kila mchezaji yupo tayari kuhakikisha ushindi unapatikana.

Kapombe ameweka wazi kuwa hatujapata ushindi dhidi yao kwenye mechi kadhaa tulizokutana nao lakini hiyo imebaki kuwa historia na leo ni siku mpya na tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

"Tunajua tuna jukumu zito kuelekea mchezo huu kutokana na kupoteza mechi nyingi dhidi yao lakini tumejipanga kuhakikisha tunajirekebisha na kupata alama tatu kwakuwa malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu," amesema Kapombe.

Nyota sita kucheza Dabi ya kwanza leo...

Nyota wetu sita tuliowasajili kwenye dirisha dogo la usajili la mwezi Januari watacheza mechi yao ya kwanza ya Dabi ya Kariakoo leo.

Nyota hao Mamadou Djibrilla Kassali, Ismail Toure, Libasse Gueye, Anicet Oura, Inno Jospin Loemba na Baraka Mwangosi.

Kwa upande wa Clatous Chama licha ya kujiunga kwenye dirisha hilo hilo lakini alishacheza Dabi nyingi huko nyuma huku Nickson Kibabage akicheza lakini kipindi hicho alikuwa upande wa pili.

Back to homepage
Share this story