Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu chanya ya ushindi wa bao moja tuliopata katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa kwenye mji wa FrancisTown nchini Botswana wiki iliyopita.
Pamoja na ushindi huo tuliopata ugenini bado tutaingia kwenye mchezo wa leo kwa tahadhari na kuwaheshimu Gaborone kwakuwa malengo yetu ni kushinda ili tuweze kusonga mbele.
Morocco atoa ahadi kwa Wanasimba......
Kaimu kocha mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco' ametoa ahadi kwa wapenzi na mashabiki wa klabu kuwa leo watafurahi na kuvuka hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa Gaborone ingawa haitakuwa mechi rahisi.
Morocco ameweka wazi kuwa wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tayari kwa kuipigania timu ili kupata matokeo chanya ambayo yataivusha na kutinga hatua inayofuata.
"Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo, na ninachotaka kuwaambia ni kwamba popote mtakapokuwa tumejiandaa kuwapa furaha. Tuna kikosi kizuri ambacho tunaamini kitaweza kutuvusha," amesema kocha Morocco.
Kikosi kipo tayari Kapombe afunguka.....
Nahodha wa timu, Shomari Kapombe amesema wachezaji wote wapo tayari kufuata maelekezo watakayopewa na walimu ili kupatikana kwa ushindi kwenye mchezo wa leo.
Kapombe amesema tunategemea kupata upinzani mkubwa na kwa namna yoyote hatutaidharau Gaborone kwakuwa lengo letu ni moja kushinda na kutinga hatua inayofuata.
"Kwa upande wetu wachezaji tupo kamili kwa ajili ya mchezo, malengo yetu ni kufika hatua za mbele na ili kufanikisha lazima hilo lazima tushinde mechi hizi za awali," amesema Kapombe.
Bajaber kuukosa mchezo wa leo
Kiungo mshambuliaji Mohamed Bajaber ataendelea kukosekana kwenye kikosi kutokana na kuuguza jeraha ingawa hali yake imezidi kuimarika na atarejea dimbani siku chache zijazo.