Jana jioni kikosi kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Mo Simba Arena na wachezaji wote wameshiriki mazoezi hayo.
Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Mtibwa lakini hata hivyo tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika Uwanja wa nyumbani.
Kauli ya Kocha Barker....
Kocha Mkuu, Steve Barker amesema Simba ni timu kubwa na mara zote inapambana kwa ajili ya ubingwa hivyo ili kutimiza hilo lazima kupata ushindi kwenye kila mchezo na hilo ni moja ya malengo yetu.
Barker amesema kurejea kwa wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa kumeongeza nguvu na kunalipa wigo mpana benchi la ufundi kufanya uchaguzi wa kikosi kwenye mchezo wa leo.
"Tupo tayari kwa mchezo, wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tayari kwa mechi ambayo tunafahamu itakuwa ngumu. Tumejipanga kuhakikisha tunashinda kwakuwa malengo yetu ni kupigania ubingwa," amesema Barker.
Wachezaji wapo tayari.......
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mkabaji, Daud Semfuko amesema kwa upande wao wapo tayari kuhakikisha wanapambana mpaka mwisho na kufuata maelekezo watakayopewa na walimu ili alama tatu muhimu zipatikane.
"Kwa upande wetu kama wachezaji tupo tayari, kila atakayepata nafasi ya kucheza atakuwa tayari kuipigania timu kupata matokeo na hilo ndilo lengo kuu," amesema Semfuko.
Morice arejea kikosini....
Kiungo mshambuliaji Morice Abraham ambaye alipata maumivu akiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa amerejea kikosini na jana ameshiriki mazoezi ya mwisho na kama kocha, Barker ataona inafaa anaweza kumtumia.
Mechi ya kwanza ya Barker....
Mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa utakuwa wa kwanza wa Ligi Kuu kwa kocha mkuu Steve Barker pamoja na benchi lake la ufundi kukiongoza kikosi.