Simba Sports Club
News

Tupo tayari kuimaliza kazi tuliyoianza Eswatini

26 Oct 2025

Tutaingia kwenye mchezo wa pili tukiwa na kumbukumbu chanya kufuatia ushindi wa mabao 3-0 tuliopata kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa Jumapili iliyopita nchini Eswatini.

Pamoja na ushindi huo ambao umetuweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi bado tutaingia kwa tahadhari kwakuwa tunahitaji kufikia malengo tuliyojiwekea.

Kazi Bado haijaisha.....

Kocha msaidizi, Seleman Matola ameweka wazi kuwa bado hatujamaliza kazi kwakuwa kuna dakika 90 leo ambazo lolote linaweza kutokea ndio maana tumejipanga vilivyo ili kuweza kufikia malengo.

Matola amesema pamoja na kuwa mbele kwa idadi hiyo mabao huku tukicheza nyumbani lakini hatutabweteka na tutaingia uwanjani kwa kutafuta mabao mengi zaidi.

"Tuna uzoefu mkubwa wa michuano hii, tumewahi kuwa kwenye hali kama hii lakini sasa tumejidhatiti vizuri. Ni kweli tunaongoza kwa mabao matatu lakini bado hatujafuzu," amesema Matola.

Kapombe atoa neno......

Advertisement

Nahodha wa timu, Shomari Kapombe amesema wachezaji wapo tayari kuhakikisha ushindi unapatikana huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi.

Kapombe amesema itakuwa mechi ngumu kwakuwa Nsingizini watakuja kwa kasi huku wakijua hawana cha kupoteza lakini tumejipanga vizuri kwa ajili ya kuwakabili.

"Haitakuwa mechi rahisi, wapinzani wetu ni timu nzuri na tunategemea watakuja kivingine hasa ukiangalia matokeo ya mchezo wa kwanza yalivyokuwa lakini sisi tupo tayari kuwakabili," amesema Kapombe.

Kante arejea, Camara bado.....

Kiungo mkabaji, Allasane Kante ambaye alikosekana kwenye mchezo wa kwanza kutokana nakuwa majeruhi amerejea na yupo tayari kwa mchezo wa leo.

Kwa upande wake mlinda mlango Moussa Camara yeye bado anaendelea na matibabu na hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani leo.

Back to homepage
Share this story