Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya kufungana bao moja na Mtibwa Sugar katika mchezo uliopita.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu, mara zote tulizokutana na Mashujaa wametupa upinzani mkubwa.
Kocha Barker atia neno....
Kocha Mkuu, Steve Barker amesema wachezaji wapya wanaingia pole pole kwenye kikosi na maendeleo ya timu kwa ujumla yanaridhisha kitu ambacho kinatupa matumaini ya kupata matokeo chanya kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa.
Barker ameongeza kuwa amefanikiwa kutazama baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya NBC na amebaini timu nyingi zimejiandaa na zina wachezaji wazuri ndio maana tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri.
Aidha Barker ameongeza kuwa malengo ya Simba ni kupambana kwa ajili ya kupata ubingwa ndio maana kila mchezo tumeupa umuhimu mkubwa.
"Maendeleo ya timu yanaridhisha kila baada ya mechi tunayocheza unaona mabadiliko makubwa ya kiuchezaji hilo linatupa matumaini. Tunategemea kuwapa furaha mashabiki wetu," amesema kocha Barker.
Wachezaji wapo tayari.......
Kwa upande wake kiungo mkabaji, Daud Semfuko amesema kila mchezaji anajua umuhimu wa alama tatu katika mechi ya kesho hasa kutokana matokeo yasiyoridhisha katika michezo yetu iliyopita.
"Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha ushindi unapatikana, hata sisi tunaumia kwa matokeo tunayopata lakini tumejipanga kujitoa mpaka mwisho ili kuweza kuwapa furaha mashabiki," amesema Semfuko.