Ni mchezo ambao tunahitaji kupata matokeo ya ushindi ili kuweza kurejesha matumaini ya kusonga mbele hatua ya robo fainali.
Tutaingia katika mchezo tukiwa tunafahamu kuwa utakuwa mgumu kwakuwa hata wapinzani wetu ES Tunis nao hawapo kwenye nafasi katika msimamo lakini tumejipanga kuwakabili.
Barker anaamini kikosi chake....
Kocha Mkuu, Steve Barker amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na kila timu kuhitaji alama tatu kwa sababu kila moja haipo nafasi nzuri kwenye msimamo ingawa tumejiandaa vizuri.
Akizungumzia hali ya kikosi, Barker amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na morali zipo juu tayari kuhakikisha malengo ya timu yanafikiwa.
"Utakuwa mchezo mgumu kwa timu zote kutokana nafasi tulizopo haziridhishi, lakini sisi tumekuja na malengo ya kuhakikisha tunashinda ili kufufua matumaini ya kusonga mbele," amesema kocha Barker.
Wachezaji wapo tayari....
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Rushine De Reuck amesema pamoja na kutoanza vizuri kwenye mechi zetu mbili za mwanzo lakini hatujakata tamaa na tupo tayari kupambana ili kupatikana kwa alama tatu.
"Bado tuna matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho, tunafahamu itakuwa mechi ngumu na tunawaheshimu wapinzani wetu lakini tumekuja kushindana ili kupata matokeo mazuri," amesema De Reuck.
Wanne kucheza kwa mara ya kwanza
Wachezaji wetu watano tuliowasajili katika dirisha dogo la Januari ni miongoni mwa nyota 22 ambao wapo kikosini kwa ajili ya mchezo wa leo.
Nyota hao ni mlinda mlango, Mamadou Djibrilla Djibo, Ismail Toure, Libasse Gueye na Nickson Kibabage ambao wataonekana kwa mara ya kwanza wakiwa na jezi ya Simba.
Kwa upande wa Clatous Chama yeye ni mzoefu kwenye kikosi ingawa kwa leo itakuwa mechi yake ya kwanza tangu kurejea kwake.