Baada ya kushindwa kuendelea mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tunaelekeza nguvu katika Ligi Kuu pamoja na CRDB Federation Cup.
Mchezo wa leo dhidi ya KMC ni muhimu kwetu kupata ushindi kwakuwa malengo yetu yote kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda taji la Ligi msimu huu.
Barker afunguka.......
Kocha Mkuu, Steve Barker amesema wachezaji wanaonyesha jitihada kubwa ya kuhakikisha timu inarejea katika hali yake ya ushindi kwenye kila mchezo kitu ambacho kinampa matumaini.
Kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya KMC, Barker amesema utakuwa mgumu kutokana na mpizani wetu kutokuwa kwenye hali nzuri lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo chanya.
Barker ameongeza kuwa haitakuwa mechi rahisi licha ya KMC kuwa mkiani mwa msimamo ndio maana tumeweka nguvu kubwa kuhakikisha tunapata ushindi.
"Tupo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya KMC, wachezaji wapo kwenye hali nzuri na kikosi kinazidi kuimarika kila siku na matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa," amesema Barker.
Wachezaji wapo tayari.....
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia David Kameta 'Duchu' amesema kila mmoja anafahamu umuhimu wa kushinda mchezo wa leo pamoja na ugumu ambao tunategemea kukutana nao.
"Tunahitaji ushindi kwenye mchezo huu, hatupo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo tunahitaji kushinda ili kurejesha matumaini," amesema Duchu.