Simba Sports Club
News

Tunaanza Kampeni ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika

23 Nov 2025

Tulianza michuano hii hatua ya awali Septemba mwaka huu kwa kuitoa Gaborone United ya Botswana kabla ya kutupa mbali Nsingizini Hotspurs ya Eswatini katika hatua ya kwanza.

Asili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa kila unapozidi kusonga mbele ndio ugumu unaongezeka na hata mechi ya leo dhidi ya Petro De Luanda tunategemea kupata upinzani mkubwa.

Pamoja na upinzani na ugumu wa wapinzani wetu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kupata alama tatu muhimu nyumbani.

Matola atoa kauli kuelekea mchezo wa leo....

Kocha msaidizi, Seleman Matola amesema hatujawahi kukutana na Petro hapo kabla na tunaiheshimu kutokana na ubora walionao lakini tumejipanga na itakuwa vizuri kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza.

Matola ameongeza kuwa wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo huo huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuwapa chachu ya kutafuta alama tatu.

Advertisement

"Kikosi kipo tayari kwa mchezo wa kesho, tunafahamu haitakuwa mechi rahisi Petro ni timu imara, kuna ugumu wa kucheza na timu ambayo haujuani nayo lakini tuna uzoefu mkubwa kwenye mashindano haya na tumejipanga kufanya vizuri ili kuwapa furaha mashabiki," amesema Matola.

Wachezaji wapo tayari.....

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, kiungo mshambuliaji, Joshua Mutale amesema wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ingawa anaamini utakuwa mgumu.

"Tumepata maandalizi mazuri kutoka kwa walimu wetu na kwakifupi tupo tayari kwa mchezo hata kama utakuwa mgumu tunahitaji kupata ushindi nyumbani," amesema Mutale.

Camara, Hamza kuikosa Petro.....

Nyota wawili mlinda mlango, Moussa Camara na mlinzi wa kati, Abdulazak Hamza ndio pekee ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana nakuwa majeruhi.

Back to homepage
Share this story