Siku mbili zilizopita tulitoa msaada kama huu katika Kituo cha kukuza na kulea watoto yatima cha Ilemela kilichopo jijini Mwanza lengo likiwa ni kurejesha kwa jamii na kumuomba Mungu atusaidie kwenye mambo yetu hasa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo tutaanza Jumatano ijayo kwa kuikaribisha Bravo FC kutoka Angola.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema Simba tumekuwa na utaratibu wa kutoa misaada hasa kwenye uhitaji kwakuwa tunajua ni baraka hata kwa Mungu.
"Leo tumekuja kuwasalimu, kuwatembelea na kuwaletea zawadi ambazo zitawasaidia katika siku mbili tatu, huu ni utaratibu ambao Wanasimba wote nchi nzima wanatakiwa kufanya hivi kwakuwa ni jambo la Baraka," amesema Ahmed.
Steven Salum, Afisa Mahusiano kutoka Mo Dewji Foundation amesema Taasisi hiyo itaendelea kuwa bega bega nao na kuendelea kutoa misaada mbalimbali kwakuwa hiyo ni moja ya kazi zao.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi CPA. Issa Masoud amesema mara zote Simba ipo karibu na wenye uhitaji na malengo ni kuhakikisha tunawafikia watu wengi zaidi kwakuwa ndilo jambo ambalo hata Mungu ameliamrisha.
Nae Katibu wa Kituo cha Mwandaliwa, Omary Kyaruzi ameupongeza Uongozi wa Simba pamoja na Mo Dewji Foundation kwa msaada huo mkubwa kwa watoto huku alituombea Dua kufanya vizuri katika michuano iliyo mbele yetu hasa mchezo wa Jumatano dhidi ya Bravo.
"Sisi kama Uongozi wa Kituo tunawashukuru Simba kwakuja kutuona pamoja na kutupa misaada hii, hili ni jambo kubwa kwetu na tunawatakia kila kheri katika mashindano yenu yote mnayoshiriki," amesema Kyaruzi.