Huu ni muendelezo wa kurejesha kwa jamii kila tunapoelekea kwenye mechi zetu za Kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie kufikia malengo yetu.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally amesema lengo la misaada hiyo ni kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie malengo yetu ya kufanya vizuri lakini pia kuwapa furaha watoto yatima ambao mara nyingi wamekuwa wakisahaulika katika Jamii.
"Leo tumekuja hapa Al-Zam kwa ajili ya kutoa misaada kwa wadogo zetu na watoto wetu mliopo hapa kikubwa tunataka kuwarejeshea tabasamu, Simba siku zote itafanya kila linalowezekana ili kuwapa furaha."
"Lakini pia tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie kupata ushindi katika mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro De Luanda kutoka Angola keshokutwa Jumapili," amesema Ahmed.
Kwa upande wake Katibu wa Al-Zam, Mussa Bilal ameushukuru Uongozi wa klabu pamoja na Mo Dewji Foundation kwa msaada huo huku akiziomba Taasisi nyingine zifanye kama Simba ili kuwapa furaha watoto yatima.
"Nichukue nafasi hii kuushukuru Uongozi wa Simba kwa kutukumbuka na kutuletea msaada huu, sio tu furaha kwa watoto lakini pia mchango huu mkubwa na tunawaombea kwa Mungu mfanikiwe katika mchezo wenu siku ya Jumapili," amesema Bilal.