Try Again amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Rais wa FIFA, Gianni Infantino kuhusu michuano ya Africa Super League ambayo tutashiriki pamoja maendeleo ya soka nchini Tanzania.
Try Again amesema Rais Infantino amepongeza hatua kubwa ya maendeleo ya mpira wa miguu barani Afrika na huku akiipongeza pia Tanzania kwa jinsi ambavyo soka lake linazidi kupanda siku hadi siku.
"Nimefurahi kukutana na Rais wa FIFA, Infantino pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu, Ornella Desirée Bellia kujadili kuhusu Super League. Majadiliano yamekuwa mazuri na jambo jema Rais Infantino anaielewa vizuri Tanzania na ameniahidi atakuwepo kwenye uzinduzi wa Super League ambao utafanyika Tanzania."
"Tuko hapa Sydney kushiriki kozi ya Diploma katika Uongozi wa Klabu inayotolewa na FIFA (Diploma in Club Management) lakini pia kufanya shughuli za mpira ikiwepo kujifunza namna mashindano makubwa yanavyoandaliwa kama Kombe la Dunia la Wanawake ambalo linafanyika hapa Australia na New Zealand.
Kama mnavyofahamu Simba itashiriki katika Africa Super League hivyo uzoefu huu utatusaidia katika uandaaji wa sherehe za ufunguzi pamoja na michezo ya kimataifa iliyopo mbele yetu," amesema Try Again.