Sowah amesema kadi nyekundu aliyopata kwenye fainali ya CRDB Federation Cup akiwa na timu yake ya zamani ilikuwa ni sehemu ya mchezo lakini haimaanishi kuwa yeye hana nidhamu kama wengi wanavyodhani.
"Kupata kadi nyekundu kwa mchezaji ni kawaida, kilichonitokea ni sehemu ya mchezo lakini watu wanatumia mitandao ya kijamii kusema kuwa sina nidhamu kitu ambacho sio kweli mimi ni mtu poa sana na ninapenda amani," amesema Sowah.
Sowah ameongeza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa anahitajika na Simba alifurahi kwakuwa anafahamu anaenda kucheza timu kubwa yenye mashabiki wengi Afrika na hata familia yake ilibariki suala hilo.
Kabla ya kukubali kujiunga nasi aliwasiliana na kiungo mshambuliaji, Elie Mpanzu ambaye alimwambia kuwa kama watakubaliana na Uongozi wa klabu akubali kujiunga kwakuwa ni timu sahihi kwake.
"Baada ya kuongea na familia yangu kuhusu kutaka kujiunga Simba pia niliwasiliana na Mpanzu ambaye alinisisitiza nikubali sababu itakuwa sehemu sahihi kwangu na alikuwa anaamini katika uwezo wangu," amesema Sowah.
Nyota huyo raia wa Ghana amewaomba Wanasimba kumpa ushirikiano huku pia akiwaahidi atazidi kuwapa furaha kila atakapopata nafasi.
"Msimu uliopita niliweka rekodi ya kufunga mabao 15 katika michezo 15 na malengo yangu kuelekea msimu ujao ni kufunga zaidi kikubwa namuomba Mungu aniepushe na majeraha," amemalizia Sowah.