Simba Sports Club
News

Pablo: Mechi na Dar City kurudisha heshima kikosini

29 Jan 2022

Kocha Mkuu Pablo Franco ameweka wazi ushindi katika mchezo wa kesho wa Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Dar City ni muhimu ili kubadili hali ya hewa kikosini baada ya kutokuwa na mwenendo wa matokeo mazuri hivi karibuni.

Amesema katika siku tisa zilizopita hatukufanya vizuri kwenye ligi tukiambulia alama moja kati ya tisa kitu ambacho hakimpendezi na si kizuri kwa timu kubwa inayopigania ubingwa hivyo tunapaswa kuhakikisha tunarudi katika mstari haraka iwezekanavyo.

Akizungumzia nchezo huo Pablo amesema utakuwa mgumu kwa sababu Dar City wataingia uwanjani wakiwa hawana cha kupoteza kwa hiyo watataka kutupa presha ili kututoa mchezoni lakini tayari tumelifanyia kazi suala hilo.

Advertisement

Pamoja na mambo mengine amesema anafikiria kufanya mabadiliko kidogo ya kikosi katika baadhi ya nafasi ili kuwapa nafasi ya kupumzika nyota wengine kutokana na ratiba ngumu ndani ya kipindi kifupi.

"Tunataka kuhakikisha tunarudisha hali ya kujiamini kikosini kwa kushinda mchezo wa kesho. Hatujapata matokeo mazuri katika mechi tatu zilizopita kwahiyo tunahitaji ushindi pekee.

"Mchezo utakuwa mgumu, wapinzani hawana cha kupoteza na wanajua tuko katika kipindi kigumu kwa hiyo watataka kutupa presha ili kututoa mchezoni lakini tupo tayari kuwakabili," amesema Pablo.

Back to homepage
Share this story