Okrah amesema tangu amekuja Tanzania hajawahi kuzungumza na mwandishi au chombo chochote cha habari hivyo ameshangaa kusambaa kwa taarifa hizo ambazo amesema zina nia ovu za kumchafua ndani ya klabu.
Akizungumzia maisha yake ndani ya klabu Okrah amesema tangu ajiunge na kikosi amekuwa na furaha kwani mahitaji yake yote anapata na kama vile haitoshi, anapata muda mwingi wa kucheza kitu ambacho ndiyo muhimu katika maisha yake.
"Hata mimi nashangaa kuona taarifa hizo, sijawahi kuzungumza na chombo chochote cha habari tangu nije Simba nashangaa kuona kwenye mitandao ya kijamii kuwa sina furaha na ninataka kuondoka. Taarifa hizo si za kweli, mimi ni mchezaji wa Simba na nina furaha kuwa hapa," amesema Okrah.
Akizungumzia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Okrah amesema uwezekano wa kufanya vizuri kwenye Kundi C lenye timu za Raja Casablanca, Horoya na Vipers ni mkubwa endapo kila mmoja ndani ya klabu atatimiza majukumu yake ipasavyo.
"Tumepangwa kundi gumu lakini hakuna kinachoshindikana, tunaweza kufika mbali kama kila mtu atatimiza majukumu yake na wachezaji watacheza kwa kujituma kila mchezo," amesema Okrah.
Okrah pamoja na kikosi kizima cha Simba kipo katika maandalizi ya kuelekea Kanda ya ziwa kwa ajili ya mechi tatu za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, Geita Gold na KMC.