Mpaka sasa tumecheza mechi 27 tukiwa nafasi ya pili kwenye msimamo.
Kwenye kikosi chetu kuna wachezaji ambao wamecheza mechi nyingi ukilinganisha na wengine kutokana na machaguo ya walimu.
Hawa hapa nyota watano waliocheza mechi nyingi...
1. Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'
Mlinzi wa kushoto Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' anaongoza kuwa mchezaji aliyecheza dakika nyingi zaidi katika kikosi chetu.
Zimbwe Jr amecheza mechi 24 sawa na dakika 2,138 akiwa haijafunga lakini amesaidia kupatikana kwa mabao matano (assist).
2. Aishi Manula
Mlinda mlango Aishi Manula anashika nafasi ya pili kwenye wachezaji waliocheza dakika nyingi katika kikosi chetu.
Manula amecheza mechi 23 sawa na dakika 2,026 akiwa amecheza michezo 12 bila kuruhusu bao (clean sheet).
Kwa sasa Manula anasumbuliwa na nyonga na tayari amekosa mechi tano zilizopita.
3. Mzamiru Yassin
Kiungo mkabaji Mzamiru Yassin amekuwa muhimili mkubwa kwenye kikosi chetu msimu huu.
Mzamiru amecheza mechi 24 sawa na dakika 1,927 akifunga mabao mawili na kusaidia kupatikana kwa mengine matano (assist).
4. Henock Inonga
Mlinzi wa kati, Henock Inonga anashika nafasi ya nne ya kuwa mchezaji aliyecheza dakika nyingi ndani ya kikosi chetu.
Inonga amecheza mechi 23 sawa na dakika 1,881 akifunga mabao matatu.
5. Shomari Kapombe
Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe anashika nafasi ya tano kwa wachezaji waliocheza dakika nyingi katika kikosi chetu mpaka sasa ligi ikiwa inaelekea ukingoni.
Kapombe amecheza mechi 21 sawa na dakika 1,867 akifunga mabao mawili na kusaidia kupatikana kwa mengine sita.