Barker amesema ni mchezo muhimu kwakuwa unatoa taswira kwenye mbio za ubingwa ndio maana amewaandaa wachezaji kimwili na kiakili kuhakikisha tunapata ushindi.
Barker ameendelea kwa kusema kuwa Azam ni timu imara na inaundwa na wachezaji wengi wazoefu na kocha bora lakini tumefanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu.
Akizungumzia kuhusu hali ya wachezaji kocha, Barker amesema wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja anafahamu umuhimu wa ushindi kwakuwa malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu.
"Maandalizi ya mchezo yamekamilika, wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri. Tunategemea kupata ushindani mkubwa lakini tumejiandaa kuwakabili," amesema Barker.
Kwa upande wake nahodha wa timu, Shomari Kapombe amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja yupo tayari kwa mchezo.
Kapombe amesema tumepoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi yao lakini kesho ni siku nyingine na mpango wa mechi pamoja na wachezaji ni wengine.
"Tuna wachezaji wengi ambao hawakuwepo tulipocheza mechi ya kwanza dhidi ya Azam, na wameonyesha uwezo mkubwa, tunaamini kwa kushirikiana na sisi wazoefu tunaweza kufanya vizuri," amesema Kapombe.