Kiungo mshambuliaji Benard Morrison, amesema kabla ya kufunga goli la kusawazisha kwenye mchezo wa jana dhidi ya US Gendermarie alitaka kwenda kupiga kona lakini Shomari Kapombe alimkataza na kumwambia amuachie.
Morrison amesema baada ya kupata kona alikwenda kwa lengo la kupiga kwa sababu aliona wachezaji wengi walikuwa wamechoka akiwemo Kapombe mwenyewe lakini mlinzi huyo alimsisitiza amuachie apige.
"Nilimuona Kapombe pamoja wengine wakiwa wamechoka nikamwambia nipe mimi nipige lakini akakataa akaniambia niende ndani.
"Baada ya kufika ndani mpira uliopigwa na Kapombe ukaja pale pale nilipokuwa nimesimama nikafunga kwa kichwa. Kwa kweli nimefurahi sana kuisaidia timu yangu kupata alama moja ugenini," amesema Morrison.
Katika mchezo wa jana Morrison aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Peter Banda.