Mohamed amefunga bao hilo dakika ya 69 baada ya kupokea pasi ya Moses Phiri likiwa ni la kwanza kwake tangu ajiunge nasi kutoka Malindi SC ya Visiwani Zanzibar katika dirisha dogo la usajili mwezi Desemba.
Mohamed amesema kabla ya mchezo aliongea na wazazi wake na walimtabiria kuwa kama atapangwa atafunga na ndicho kilichotokea.
"Nimefurahi sana kufunga bao langu la kwanza nikiwa na Simba. Na hili nawazawadia wazazi wangu, kabla ya mchezo waliniambia kama nikipangwa nitafunga na ndicho kilichotokea.
"Pia nimefurahi kufunga kwenye mechi kubwa ya mtoano, imeniongezea morali ya kuzidi kupambana kuisaidia timu," amesema Mohamed.
Akizungumzia nafasi yake kikosini, Mohamed amesema "naamini nitapata nafasi ya kucheza Mwenyezi Mungu ni mkubwa, ushindani upo lakini nitapambana."