Kiungo mkabaji Jonas Mkude, amewaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi katika mchezo wetu wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakaopigwa Ijumaa saa 10 jioni Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Mkude amesema ili timu ifanye vizuri unahitajika mshikamano baina ya watu wote kuanzia uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki.
Kiungo huyo mwandamizi ameongeza kuwa anafahamu mchezo utakuwa mgumu lakini wao kama wachezaji wako tayari kuhakikisha wanapambana kupata alama tatu.
Mkude amesema baada ya kushindwa kucheza mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar kutokana na wachezaji kuugua jopo la madaktari limefanya kazi kubwa na sasa kila kitu kiko sawa tayari kuwavaa KMC.
"Ninawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani Ijumaa, sisi wachezaji tupo tayari kupambana kuhakikisha tunawapa furaha.
"Kiafya wachezaji wote tuliopo hapa tuko fiti na tumefanya mazoezi kwa ajili ya mchezo tunaamini kwa sapoti ya mashabiki wetu tutaibuka na ushindi," amesema Mkude.