Kocha mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi ameweka wazi malengo yetu kuelekea kuanza msimu mpya wa mashindano 2026/2027 ni kutwaa ubingwa wa ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Mgosi amesema msimu uliopita tulitwaa ubingwa bila kupoteza mchezo huku tukitoka sare mechi tatu lakini sasa tunataka tusipoteze na pia tupunguze idadi ya sare.
Kuhusu mchezo wa kesho wa kwanza wa ligi dhidi ya Kilimanjaro Wanderers utakaopigwa Uwanja wa Ushirika Moshi saa 10 jioni, Mgosi amesema utakuwa mgumu lakini tumejipanga na tupo tayari kuanza kwa kupata alama tatu ugenini.
"Malengo yetu ni yale yale, kutwaa ubingwa bila kupoteza kama msimu uliopita. Tunafahamu upinzani utakuwa mkubwa lakini tumejipanga kwa kuanza kampeni ya kutetea taji letu," amesema Mgosi.
Kwa upande wake nahodha wa timu, Fatuma Issa 'Fetty Densa' amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri morali zipo juu kuelekea mchezo wa kesho.
"Sisi kama wachezaji tupo tayari na kwetu kila mchezo ni fainali lengo ni kuhakikisha tunapambana kwa ajili ya alama tatu," amesema Fetty Densa.