Kikosi kimefanya mazoezi ya kawaida asubuhi kwa mujibu wa programu na jioni wameingia gym ili kuendelea kutengeneza utimamu wa mwili.
Mshambuliaji Moses Phiri ambaye amekosa mechi za mwisho za msimu uliopita kutokana na majeraha amepona na yupo kamili kama wachezaji wengine na anaendelea na mazoezi.
Akizungumzia hali ya Phiri, Daktari wa timu Edwin Kagabo amesema kwa sasa yupo kamili kabisa sawa na wachezaji wengine na anatimiza majukumu yake uwanjani kwa asilimia 100.
"Phiri amerejea vizuri na amekuwa kwenye hali nzuri kama ilivyokuwa mwanzo wa msimu, kuhusu wachezaji wengine wote waliyopo hapa kambini kila mmoja yupo sawa kiutimamu wa mwiili ndio maana wanaendelea na mazoezi hakuna mwenye shida yoyote," amesema Dk. Kagabo.
Kwa upande Phiri mwenyewe amesema "Namshukuru Mungu nimerejea nikiwa sawa kiafya na akili tofauti na ilivyokuwa mwishoni mwa msimu uliopita, nafanya mazoezi pamoja na wenzangu kilichobaki ni kuendelea na maandalizi ili kwenda kutoa mchango msimu ukianza na kufikia malengo yetu."