Kikosi chetu kiko njiani kuelekea nchini Sudan kutokana na mwaliko kutoka kwa Al Hilal kushiriki michuano maalumu ya kujiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa ikiwa ni sehemu ya ushirikiano baina yetu.
Matola amesema mechi mbili dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na wenyeji Al Hilal itakuwa ni kipimo sahihi kutokana na kuwa ni mabingwa wa nchi zao na wazoefu wa michuano ya Afrika.
Matola ameongeza kuwa wachezaji wapo kwenye hali nzuri isipokuwa kiraka Erasto Nyoni amebaki kutokana na kuugua Malaria ambapo anaungana na wale tisa walioitwa timu ya taifa ya Tanzania.
"Ukiangalia Kotoko ni Mabingwa wa Ghana, Hilal ni mabingwa wa Sudan na wana uzoefu mkubwa kwenye michuano ya Afrika, tunaamini tutapata mazoezi mazuri kuelekea mechi yetu dhidi ya Bullets.
"Tumemuacha Erasto kutokana na kuugua Malaria lakini wachezaji wengine wapo vizuri na tumesafiri nao," amesema Matola.
Kikosi kimeondoka nchini alfajiri kuelekea Sudan tukiwa na wachezaji 18 benchi zima la ufundi na viongozi.