Kocha msaidizi, Seleman Matola amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo FC yamekamilika na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri.
Matola amesema kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri na jana kimefanya mazoezi baada ya kurejea kutoka Manyara na hakuna mchezaji aliyepata maumivu ambayo yanaweza kumfanya kuukosa mchezo wa kesho.
Matola ameweka wazi kuwa tunaenda kukutana na timu ngumu yenye kocha bora na haijawahi kuwa mechi nyepesi kila tunapokutana na Namungo lakini tumejiandaa kuhakikisha tunapata alama tatu.
"Maandalizi ya mchezo wa kesho yanaendelea vizuri wachezaji wapo kwenye hali nzuri. Namungo ni timu imara inayoundwa na wachezaji wazuri pamoja na mwalimu wao lakini pamoja na ugumu wao lengo letu ni kuhakikisha tunapata alama zote," amesema Matola.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto, Anthony Mligo amesema kila mchezaji anafahamu kuwa lengo letu kuu msimu huu ni kutwaa ubingwa wa ligi hivyo kila mechi kwetu ni fainali.
"Msimu huu Simba tuna malengo makubwa, tunahitaji kutwaa ubingwa wa ligi hivyo tunatakiwa kushinda kila mechi ili kuweza kuyafikia malengo hayo."
"Sisi wachezaji tunajua tunaenda kukutana na timu ngumu ya Namungo lakini tumejiandaa kuhakikisha tunashinda mchezo huo ili kuendelea kuyasogelea malengo yetu," amesema Mligo.