Simba Sports Club
News

Matola aumizwa na shutuma za mashabiki

2 Nov 2022

Matola amesema mara zote timu inapofungwa au kupata sare mashabiki huanza kumtolea maneno ya kejeli kuwa yeye ndiyo chanzo cha matokeo hayo wakati ikifanya vizuri wanakuwa kimya.

Akizungumza na Simba App, Matola amesema hazuii watu kumlaumu kwani kazi ya mpira ni kazi ya lawama lakini kama binadamu anaumizwa na kuchoshwa na lawama zote zinazoelekezwa kwake kila wakati.

"Haiwezekani mashabiki wanigeuze mimi kichaka cha lawama tena wakati mwingine wananipa tuhuma za kuhujumu timu inawezekana vipi mimi nikahatarisha kibarua changu kwa kuhujumu kazi yangu.

“Mimi nina ndoto za kuwa kocha mkubwa Afrika, siwezi kuingia kwenye kashfa za kuhujumu kazi yangu ninayoitegemea” amesema Matola

Advertisement

Kwa upande wake Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amesema uongozi una imani kubwa na Kocha Matola na amekuwa nguzo muhimu ya kuisaidia klabu.

Ameongeza kuwa tuhuma zote dhidi ya Matola hazina uhalisia na hivyo amewataka mashabiki kumpa heshima kocha huyo ambaye amejitoa maisha yake yote kwa ajili ya Simba.

"Kocha Selemani Matola ameanza kuhudumu Simba kama mchezaji, kocha wa timu za vijana kabla ya kukabidhiwa jukumu la kocha msaidizi wa timu ya wakubwa," amesema Ahmed.

Back to homepage
Share this story