Matola amesema mwaka 2003 baada ya kuwatoa Zamalek ya Misri tulikutana na ASEC katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mtanange ambao ulikuwa mgumu na kuvutia.
Matola ambaye kipindi hicho alikuwa nahodha wa kikosi chetu amesema kuelekea mchezo huo timu ilipata maandalizi makubwa na kambi iliwekwa katika Hotel ya Silver Sand jijini Dar es Salaam ambayo ilikuwa maarufu ili wachezaji wapate utulivu.
Kiungo huyo mkabaji ameongeza kuwa katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam tuliibuka na ushindi wa bao moja na tulivyokwenda kwao kwa marudiano tukapoteza kwa mabao 4-3.
"Mechi ilikuwa ngumu sana, nakumbuka hata maandalizi yake yalikuwa makubwa. Tulikaa kwenye hoteli nzuri na kila kitu kilikwenda vizuri.
"Tulishinda nyumbani na tulihitaji ushindi ili tufuzu robo fainali lakini haikuwa hivyo, tulipoteza kwa mabao 4-3 lakini mechi ilikuwa ngumu. Baada ya mchezo tulijipongeza kwa kazi tuliyofanya kwa sababu ASEC ilikuwa timu bora sana kipindi hicho," amesema Matola.