Mlinda mlango namba moja Aishi Manula, amesema tutachukua tahadhari zote katika mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane utakaopigiwa Jumapili saa 10 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Manula amesema mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kubaki na alama zote tatu nyumbani.
Manula amesema malengo ni kuhakikisha tunachukua alama tatu bila kisingizio chochote ingawa haitakuwa kazi rahisi kuwafunga miamba hiyo ya Morocco.
"Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu, Berkane ni timu bora lakini tupo nyumbani na tunahitaji kushinda na tumejiandaa kikamilifu kwa jambo hili," amesema Manula.
Mlinda mlango huyo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumapili kutoa sapoti kwa wachezaji ili lengo la ushindi litimie.
"Mashabiki ni watu muhimu sana na tunawahitaji katika mchezo wa wa Jumapili. Tupo nyumbani na tunahitaji alama tatu ambazo zitatuweka katika nafasi nzuri, ujio wao utatuongezea morali uwanjani," amesema Manula.