Zoezi hilo limeanzia Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuelekea Temeke, Tandika, Mtoni kwa Azizi Ally mpaka Mbagala Zakhem.
Kama kawaida lengo la hamasa ni kuhakikisha Wanasimba wanajitokeza kwa wingi uwanjani Jumapili ili kuisapoti timu kufanya vizuri na kufuzu hatua ya makundi.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amewasisitiza Wanasimba kununua tiketi kwa wingi ili kuujaza Uwanja kama walivyofanya wapinzani wetu nyumbani kwao.
"Leo hatuna mambo mengi ya kuzungumza zaidi ya kuwahamaisha Wanasimba mje kwa wingi Jumapili ili kwa pamoja tukaisaidie timu yetu kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho," amesema Ahmed.
Saa nane mchana watu hamasa wakiongozwa na Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally wameshiriki chakula cha mchana katika Kituo cha watoto yatima cha Hiari kilichopo Mbagala ikiwa ni sehemu ya kurejesha kwa jamii.
Chakula cha mchana kimekuwa zoezi la mwisho kwa siku ya leo katika muendelezo wa hamasa kuelekea mchezo wetu wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli.