Robertinho atawasili Brazil kesho na atakuwa huko kwa wiki moja kuendelea na masomo yake na baada ya kumalizika atarejea Uturuki Julai, 24 kujiunga na timu na kuendelea na programu za mazoezi.
Robertinho ameondoka lakini ameacha programu ya mazoezi chini wasaidizi wake , Ouanane Sellami na Corneille Hategekimana ambao wataongoza mazoezi kwa siku zote ambazo hatakuwepo.
Mratibu wa kikosi, Abbas Ally amesema kabla ya Robertinho kuondoka amekaa na kuzungumza na wasaidizi wake masuala ya kiufundi na kile ambacho wanapaswa kukifanyika kwa muda wote ambao hatakuwepo.
Abbas ameongeza kuwa jambo zuri kabla ya kufika Uturuki tayari Robertinho alikuwa amendaa programu yote ya mazoezi na kila kitu cha kiufundi kitakachofanyika kwahiyo hata kuondoka kwake si tatizo kwani kila kitu kipo kwenye mstari.
"Kambi yetu ipo katika hali nzuri morali za wachezaji zipo juu na kadri siku zinavyozidi kwenda wanazidi kushika mafunzo wanayopewa.
"Tunafanya kila tunachohitaji kwa wakati na ushirikiano mkubwa wa wachezaji pamoja na benchi la ufundi tunaamini tukimaliza kambi tutakuwa tumepata tulichokuwa tunahitaji," amesema Abbas.