Mshambuliaji Kibu Denis ameweka wazi kuwa endapo ikitokea akafanikiwa kufunga katika mchezo dhidi ya Mbeya City hatashangilia.
Msimu uliopita Kibu alikuwa nyota wa Mbeya City akiibuka kinara wa ufungaji wa timu hiyo na itakuwa mara ya kwanza kukutana na waajiri wake hao wa zamani hivyo amepanga kuwapa heshima.
Kibu amesema unapofunga bao katika mchezo hasa unapokuwa mgumu furaha huwa kubwa na kushangilia kwa hisia kali, hivyo ikitokea akafunga atajitahidi kutofanya hivyo na atatoa ishara ya kuomba radhi.
"Kama ikitokea leo nikapangwa na kufanikiwa kufunga nadhani sitashangilia sana. Sijui nitakuwa katika hali gani kwa muda huo kutokana na hisia lakini kama ikitokea nikashangilia itakuwa kidogo tu.
"Mbeya City ni timu nzuri, wanapambana sana na tunawaheshimu. Tunatarajia kupata ushindani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda," amesema Kibu.