Mshambuliaji Kibu Denis ameweka wazi furaha yake ya kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa kwa ngazi za klabu katika mchezo wa jana wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.
Kibu ambaye usajili wake wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ulichelewa hivyo hakuweza kucheza mechi za awali pia amepona majeraha aliyokuwa anauguza na jana ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza mechi za Afrika.
Kibu amesema kila mchezaji furaha yake ni kucheza mechi kubwa za Afrika kama ilivyokuwa jana na anaamini ataendelea kuaminiwa na kocha katika michezo inayokuja.
"Ni furaha kubwa kwangu kucheza mechi yangu ya kwanza ya kimataifa ya mashindano kwa ngazi ya klabu. Kila mchezaji anatamani kupata nafasi ya kucheza michuano hii, naamini mwalimu ataendelea kunipa nafasi," amesema Kibu.
Kibu alipata maumivu katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya City uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Januari 16 yaliyomuweka nje kwa takribani wiki saba.