Kazi ambaye tumemsajili katika dirisha hili kutoka Geita Gold amesema anaendelea kujifunza mambo mambo mengi kutoka kwa wachezaji aliowakuta.
Mlinzi huyo ameenda mbali na kusema kuwa kazi yake ni kucheza mpira na ndiyo iliyomfikisha hapa kwa hiyo hana presha huku akikiri Simba ni timu kubwa.
"Mimi naamini siku yangu itafika na nitapata namba katika kikosi cha Simba. Hayo ni malengo yangu na ninazidi kuyapigania.
"Kwa muda mfupi niliokaa hapa nimejifunza mambo mengi kutoka kwa kaka zangu niliowakuta, itanisaidia nitakapopata nafasi," amesema Kazi.
Kazi amesema kwa sasa anaelekeza nguvu katika kusaidia timu kufikia malengo iliyojiwekea ya kushinda mataji yote ya ndani pamoja na kuvuka Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Sina malengo binafsi, kwa sasa ni timu kwanza, tunahitaji kushinda mataji yote ya ndani pamoja na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika," amesema Kazi.